Isa. 22:10-16 Swahili Union Version (SUV)

10. Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.

11. Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.

12. Siku hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung’oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia;

13. na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng’ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.

14. Na yeye BWANA wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, BWANA wa majeshi.

15. Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie,

16. Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!

Isa. 22