Isa. 21:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Ufunuo juu ya bara ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka bara, toka nchi itishayo.

2. Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote.

3. Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona.

4. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha.

5. Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta.

6. Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze.

7. Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza.

8. Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu.

Isa. 21