1. Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi.
2. Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu.
3. Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari.
4. Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; BWANA wa majeshi anapanga jeshi kwa vita;
5. watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, BWANA na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote.
6. Pigeni kelele za hofu; maana siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.
7. Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka.
8. Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.