17. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja.
18. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa.
19. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.
20. Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea BWANA, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli.
21. Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu.
22. Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki.
23. Kwa maana Bwana, BWANA wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote.
24. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri.
25. Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza.
26. Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.
27. Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.
28. Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi;
29. wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia.
30. Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi!