Isa. 1:16-31 Swahili Union Version (SUV)

16. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

17. jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.

18. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.

19. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;

20. bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.

21. Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!

22. Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.

23. Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.

24. Kwa hiyo, asema Bwana, BWANA wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitatwaa kisasi kwa adui zangu;

25. nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote;

26. nami nitarejeza upya waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu.

27. Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.

28. Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao BWANA watateketezwa.

29. Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua.

30. Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji.

31. Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima.

Isa. 1