Isa. 1:11-22 Swahili Union Version (SUV)

11. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng’ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume.

12. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?

13. Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.

14. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.

15. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

16. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

17. jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.

18. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.

19. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;

20. bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.

21. Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!

22. Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.

Isa. 1