3. Mimi namjua Efraimu, wala Israeli hakufichwa nisimwone; maana sasa, Ee Efraimu, umefanya uzinzi; Israeli ametiwa unajisi.
4. Matendo yao hayatawaacha kumgeukia Mungu wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui BWANA.
5. Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; kwa sababu hiyo, Israeli na Efraimu watajikwaa katika uovu wao. Yuda naye atajikwaa pamoja nao.
6. Watakwenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe wamtafute BWANA; lakini hawatamwona; amejitenga nao.
7. Wametenda kwa hila juu ya BWANA; maana wamezaa wana wageni; sasa mwezi huu uandamao utawala pamoja na mashamba yao.
8. Pigeni tarumbeta katika Gibea, na baragumu katika Rama; pazeni sauti ya hofu katika Beth-Aveni; nyuma yako, Ee Benyamini!
9. Efraimu atakuwa ukiwa siku ya kukemewa; katika kabila za Israeli nimetangaza habari itakayotokea halafu bila shaka.
10. Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji.