13. Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake.
14. Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa BWANA; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi.
15. Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi.
16. Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku.
17. Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao.
18. Kwa amri ya BWANA Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya BWANA walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao.