1. Ilikuwa siku hiyo Musa alipokwisha kuisimamisha maskani, na kuitia mafuta, na kuitakasa, na vyombo vyake vyote, na hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote, na kuvitia mafuta, na kuvitakasa;
2. ndipo wakuu wa Israeli, vichwa vya nyumba za baba zao, wakatoa matoleo; hao ndio wakuu wa kabila, hao ndio waliokuwa juu yao waliohesabiwa;
3. nao wakamletea BWANA matoleo yao, magari sita yenye mafuniko juu, na ng’ombe kumi na wawili; gari moja kwa wakuu wawili wawili, na ng’ombe mmoja kwa kila mkuu; nao wakayasongeza hapo mbele ya maskani.
4. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
5. Pokea mikononi mwao, ili kwamba viwe vya kutumiwa katika utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawapa Walawi vitu hivyo, kila mtu utampa kama utumishi wake ulivyo.
6. Basi Musa akapokea hayo magari, na ng’ombe, akawapa Walawi.
7. Wana wa Gershoni akawapa magari mawili na ng’ombe wanne, kama utumishi wao ulivyokuwa;
8. na wana wa Merari akawapa magari manne na ng’ombe wanane kama utumishi wao ulivyokuwa, chini ya mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni kuhani.
9. Lakini hakuwapa wana wa Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao wakavichukua mabegani mwao.