18. kisha kuhani atamweka mwanamke mbele za BWANA, naye atazifungua nywele za kichwani mwa huyo mwanamke, kisha atampa hiyo sadaka ya unga ya ukumbusho mikononi mwake, ambayo ni sadaka ya unga ya wivu, naye kuhani atakuwa na hayo maji ya uchungu yaletayo laana mkononi mwake;
19. tena kuhani atamwapisha huyo mwanamke, naye atamwambia mwanamke, Kwamba hakulala mtu mume pamoja nawe, tena kwamba hukukengeuka kuandama uchafu, uli chini ya mumeo, maji haya ya uchungu yaletayo laana yasikudhuru;
20. lakini kwamba umekengeuka uli chini ya mumeo, na kwamba u hali ya unajisi, na mtu mume amelala nawe, asiyekuwa mumeo;
21. hapo ndipo kuhani atamwapisha mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, kisha kuhani atamwambia huyo mwanamke maneno haya, BWANA na akufanye wewe uwe laana na kiapo kati ya watu wako, hapo BWANA akufanyapo paja lako kupooza, na tumbo lako kuvimba;
22. na maji yaletayo laana yatakuingia matumboni mwako, na kukuvimbisha tumbo, na kukupoozesha paja lako; na mwanamke ataitika, Amina, Amina.
23. Kisha kuhani ataziandika laana hizo ndani ya kitabu, na kuzifuta katika maji ya uchungu;
24. kisha atamnywesha mwanamke hayo maji ya uchungu yaletayo laana; nayo maji yaletayo laana yataingia ndani yake, nayo yatageuka kuwa uchungu.
25. Kisha kuhani ataitwaa hiyo sadaka ya unga ya wivu, kwa kuiondoa mkononi mwa huyo mwanamke, naye ataitikisa sadaka ya unga mbele ya BWANA, na kuisongeza pale madhabahuni;
26. kisha kuhani atatwaa konzi moja ya sadaka ya unga, kuwa ni ukumbusho wake, na kuuteketeza madhabahuni, baadaye atamnywesha mwanamke hayo maji.