3. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi hata umri wa miaka hamsini, wote waingiao katika utumishi huo, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.
4. Huu ndio utumishi wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania, katika vile vyombo vitakatifu sana;
5. hapo watakapong’oa safari, Haruni ataingia ndani, na wanawe, nao watalishusha pazia la sitara, na kulifunika sanduku la ushahidi kwa hilo pazia;
6. kisha atatia juu yake ngozi za pomboo za kulifunikia, na kutandika juu yake nguo ya rangi ya samawi tupu, kisha watatia hiyo miti yake.
7. Tena juu ya meza ya mikate ya wonyesho watatandika nguo ya rangi ya samawi, na kuweka juu yake sahani, na miiko, na mabakuli, na vikombe vya kumiminia; na hiyo mikate ya daima itakuwa juu yake;
8. nao watatandika juu yake nguo ya rangi nyekundu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo za kuifunikia, na kuitia ile miti yake.
9. Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake;
10. nao watakitia, na vyombo vyake vyote, ndani ya ngozi ya pomboo, na kukitia juu ya miti ya kukichukulia
11. Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake;
12. kisha watavitwaa vile vyombo vyote vya utumishi wavitumiavyo katika mahali patakatifu, na kuvitia katika nguo ya rangi ya samawi, na kuvifunika kwa ngozi za pomboo, na kuvitia juu ya miti ya kuvichukulia.
13. Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;
14. nao wataweka vyombo vyake vyote juu yake ambavyo wavitumia katika madhabahu, vyetezo, na nyuma, na miiko, na mabakuli, vyombo vyote vya hiyo madhabahu; nao watatandika juu yake ngozi za pomboo, na kutia miti yake mahali pake.
15. Na Haruni na wanawe watakapokwisha kupafunika mahali patakatifu, na vyombo vyote vya mahali patakatifu, hapo watakapong’oa kambi; baadaye, wana wa Kohathi watakuja kuvichukua; lakini wasiviguse vile vitu vitakatifu, wasife. Vyombo vile ni mzigo wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania.
16. Na ulinzi wake Eleazari mwana wa Haruni kuhani utakuwa ni kuyaangalia mafuta kwa nuru, na uvumba mzuri, na sadaka ya unga ya daima, na mafuta ya kupaka, tena ulinzi wa hiyo maskani yote, na wa vitu vyote vilivyo ndani yake, mahali patakatifu, na vyombo vyake.