1. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2. Katika wana wa Lawi uitenge hesabu ya wana wa Kohathi, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,
3. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi hata umri wa miaka hamsini, wote waingiao katika utumishi huo, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.
4. Huu ndio utumishi wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania, katika vile vyombo vitakatifu sana;
5. hapo watakapong’oa safari, Haruni ataingia ndani, na wanawe, nao watalishusha pazia la sitara, na kulifunika sanduku la ushahidi kwa hilo pazia;
6. kisha atatia juu yake ngozi za pomboo za kulifunikia, na kutandika juu yake nguo ya rangi ya samawi tupu, kisha watatia hiyo miti yake.
7. Tena juu ya meza ya mikate ya wonyesho watatandika nguo ya rangi ya samawi, na kuweka juu yake sahani, na miiko, na mabakuli, na vikombe vya kumiminia; na hiyo mikate ya daima itakuwa juu yake;
8. nao watatandika juu yake nguo ya rangi nyekundu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo za kuifunikia, na kuitia ile miti yake.
9. Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake;