17. Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa.
18. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.
19. Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.
20. Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa;
21. au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye.
22. Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia,
23. au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara;
24. ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo;
25. nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu.
26. Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia;
27. na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu;
28. kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake.
29. Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote.
30. Mtu awaye yote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu hata akafa.