1. Kisha BWANA akanena na Musa katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko, akamwambia,
2. Uwaagize wana wa Israeli wawape Walawi miji wapate mahali pa kukaa, katika milki yao; pamoja na malisho yaliyoizunguka hiyo miji kotekote mtawapa Walawi.
3. Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote.
4. Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote.