1. Hizi ndizo safari za wana wa Israeli, hapo walipotoka nchi ya Misri kwa jeshi zao chini ya mkono wa Musa na Haruni.
2. Musa akaandika jinsi walivyotoka katika safari zao, kwa amri ya BWANA; na hizi ndizo safari zao kama kutoka kwao kulivyokuwa.
3. Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa mkono wa nguvu mbele ya macho ya Wamisri wote,
4. hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, BWANA aliokuwa amewapiga kati yao; BWANA akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo.
5. Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapanga katika Sukothi.
6. Kisha wakasafiri kutoka Sukothi, wakapanga Ethamu, palipo katika mwisho wa nyika.