15. Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote.
16. Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;
17. lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.
18. Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.
19. Kwa kuwa sisi hatutarithi pamoja nao huko ng’ambo ya pili ya Yordani, huko mbele; kwa sababu urithi wetu umetuangukia upande huu wa Yordani kwa mashariki.
20. Basi Musa akawaambia, Kama mtafanya jambo hili; kama mtajivika silaha, ili kutangulia mbele ya BWANA mwende vitani,
21. tena kama kila mume wa kwenu mwenye kuchukua silaha atavuka Yordani mbele ya BWANA, hata atakapokuwa amekwisha watoa adui zake mbele yake,
22. na hiyo nchi kushindwa mbele za BWANA; ndipo baadaye mtarudi, nanyi mtakuwa hamna hatia mbele za BWANA, wala kwa Israeli; na nchi hii itakuwa milki yenu mbele za BWANA.
23. Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za BWANA, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.
24. Basi, jengeni miji kwa ajili ya watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya kondoo zenu; mkayafanye hayo mliotamka kwa vinywa vyenu.
25. Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo.
26. Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng’ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi;