1. Basi wana wa Reubeni, na hao wana wa Gadi, walikuwa na wanyama wa mifugo wengi sana; nao walipoona nchi ya Yazeri, na nchi ya Gileadi, ya kuwa mahali hapo palikuwa ni mahali pa kuwafaa wanyama;
2. hao wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakamwendea Musa na Eleazari kuhani, na wakuu wa mkutano, wakanena nao, wakisema,
3. Atarothi, na Diboni, na Yazeri, na Nimra, na Heshboni, na Eleale, na Sebamu, na Nebo na Beoni,
4. nchi hiyo ambayo BWANA aliipiga mbele ya mkutano wa Israeli, ni nchi ifaayo kwa mfugo wa wanyama, nasi watumishi wako tuna wanyama.
5. Wakasema, Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, sisi watumishi wako na tupewe nchi hii iwe milki yetu; usituvushe mto wa Yordani.
6. Musa akawaambia wana wa Gadi na wana wa Reubeni, Je! Ndugu zenu waende vitani nanyi mtaketi hapa?
7. Mbona mwawavunja mioyo yao wana wa Israeli, wasivuke na kuingia nchi hiyo ambayo BWANA amewapa?
8. Ndivyo walivyofanya baba zenu, hapo nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea ili waende kuiangalia hiyo nchi.
9. Kwa kuwa walipokwea na kuingia bonde la Eshkoli, na kuiona nchi, wakawavunja mioyo wana wa Israeli, ili wasikwee kuingia nchi BWANA aliyowapa.
10. Na siku ile hasira za BWANA ziliwaka, naye akaapa, akisema,
11. Hakika yangu hapana mtu mmoja katika wale watu waliotoka Misri, tangu huyo aliyepata umri wa miaka ishirini, na zaidi, atakayeiona hiyo nchi niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa sababu hawakuniandama kwa moyo wote;
12. ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama BWANA kwa moyo wote.
13. Na hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa BWANA kikaisha angamia.