7. Nao wakapigana na Midiani kama BWANA alivyomwagiza Musa; nao wakamwua kila mume.
8. Nao wafalme wa Midiani wakawaua pamoja na watu wengine waliouawa; Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao wafalme watano wa Midiani; Balaamu mwana wa Beori naye wakamwua kwa upanga.
9. Wana wa Israeli wakawachukua mateka wanawake wa Midiani na watoto wao; na ng’ombe zao wote, na kondoo zao wote, na mali zao zote, wakachukua nyara.
10. Na miji yao yote, kila mahali walipokuwa wakikaa, na marago yao yote wakayateketeza kwa moto.
11. Nao wakatwaa hizo nyara zote, na mateka yote, ya wanadamu na ya wanyama.
12. Nao wakawaleta mateka ya wanadamu, na mateka ya wanyama, na hizo nyara, na kuyaweka mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wa wana wa Israeli, hapo maragoni katika nchi tambarare za Moabu, zilizo karibu na Yordani hapo Yeriko.
13. Basi Musa, na Eleazari kuhani, na wakuu wote wa huo mkutano, wakatoka nje kwenda kuwalaki nje ya marago.
14. Musa akawakasirikia majemadari wa jeshi, na hao maakida wa elfu elfu, na wakuu wa mia mia, hao waliorudi kutoka katika kupiga vita.
15. Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai?
16. Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie BWANA dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa BWANA.