5. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
6. Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia.
7. Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani.
8. Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani.
9. Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli.
10. Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.
11. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
12. Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;
13. kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi BWANA.