1. Basi vizazi vya Haruni na Musa, siku hiyo BWANA aliyosema na Musa katika mlima wa Sinai, ni hivi.
2. Tena majina ya hao wana wa Haruni ni haya; Nadabu mzaliwa wa kwanza, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.
3. Hayo ndiyo majina ya wana wa Haruni, hao makuhani waliotiwa mafuta, ambao aliwaweka wakfu ili wafanye kazi ya ukuhani.
4. Kisha Nadabu na Abihu walikufa mbele za BWANA, waliposongeza moto wa kigeni mbele za BWANA, katika bara ya Sinai, nao walikuwa hawana wana; na Eleazari na Ithamari wakafanya kazi ya ukuhani mbele ya uso wa Haruni baba yao.
5. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
6. Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia.
7. Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani.
8. Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani.
9. Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli.
10. Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.
11. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
12. Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;