2. Nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng’ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba;
3. pamoja na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa ng’ombe, sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume,
4. na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba;
5. na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu;
6. zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya kuandama mwezi, na sadaka yake ya unga, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kama ilivyo amri yake, kuwa harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto.
7. Tena siku ya kumi ya huo mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; nanyi mtazitesa nafsi zenu, msifanye kazi yo yote ya utumishi
8. lakini mtamsongezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza; ng’ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu;
9. pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa huyo ng’ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa huyo kondoo,
10. na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba;
11. na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya dhambi ya upatanisho, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji.
12. Tena siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi, nanyi mtamfanyia BWANA sikukuu muda wa siku saba;
13. nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka isongezwayo kwa moto, harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng’ombe waume wadogo kumi na watatu, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza kumi na wanne; wote watakuwa wakamilifu;
14. pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng’ombe katika wale kumi na watatu na sehemu ya kumi mbili kwa kila kondoo katika hao kondoo waume wawili;