Hes. 28:2-15 Swahili Union Version (SUV)

2. Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.

3. Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea BWANA; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.

4. Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;

5. pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.

6. Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.

7. Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia BWANA katika mahali hapo patakatifu.

8. Na mwana-kondoo wa pili utamsongeza wakati wa jioni; kama ile sadaka ya unga iliyosongezwa asubuhi, na kama sadaka yake ya kinywaji, ndivyo utakavyoisongeza, ni sadaka ya kusongezwa kwa moto, ni harufu ya kupendeza kwa BWANA.

9. Tena katika siku ya Sabato watasongezwa wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, pamoja na sehemu ya kumi mbili za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji;

10. hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila Sabato, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

11. Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea BWANA sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng’ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;

12. pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng’ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja;

13. na sehemu ya kumi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwana-kondoo; kuwa sadaka ya kuteketezwa ya harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.

14. Tena sadaka zake za vinywaji zitakuwa nusu ya hini ya divai kwa ng’ombe, na sehemu ya tatu ya hini kwa kondoo mume, na robo ya hini kwa mwana-kondoo; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika miezi yote ya mwaka.

15. Tena mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa BWANA itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

Hes. 28