1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2. Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.
3. Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea BWANA; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.
4. Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;
5. pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.
6. Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.
7. Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia BWANA katika mahali hapo patakatifu.