Hes. 27:11-19 Swahili Union Version (SUV)

11. Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa.

12. BWANA akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli.

13. Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika;

14. kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.)

15. Musa akanena na BWANA akisema,

16. BWANA, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano,

17. atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.

18. BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako;

19. kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao.

Hes. 27