Hes. 26:51-65 Swahili Union Version (SUV)

51. Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli, mia sita na moja elfu, na mia saba na thelathini (601,730).

52. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

53. Watu hawa watagawanyiwa nchi hiyo iwe urithi wao, vile vile kama hesabu ya majina yao ilivyo.

54. Hao waliozidi hesabu yao utawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka hesabu yao, utawapa urithi kama upungufu wao; kila mtu kama watu wake walivyohesabiwa, ndivyo atakavyopewa urithi wake.

55. Lakini nchi itagawanywa kwa kura; kwa majina ya kabila za baba zao, ndivyo watakavyopata urithi.

56. Kama kura itakavyokuwa, ndivyo urithi wao utakavyogawanywa kati yao, hao wengi na hao wachache.

57. Na hao waliohesabiwa katika Walawi kwa jamaa zao ni hawa; wa Gershoni, jamaa ya Wagershoni; na wa Kohathi, jamaa ya Wakohathi; na wa Merari, jamaa ya Wamerari.

58. Hizi ndizo jamaa za Lawi; jamaa ya Walibni, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya Wamala, na jamaa ya Wamushi jamaa ya Wakora. Na Kohathi alimzaa Amramu.

59. Na jina la mke wa Amramu aliitwa Yokebedi, binti wa Lawi, ambaye alizaliwa kwake Lawi huko Misri; na huyo Yokebedi akamzalia Amramu Haruni, na Musa, na Miriamu umbu lao.

60. Tena kwake Haruni walizaliwa hawa, Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.

61. Tena Nadabu na Abihu wakafa, hapo waliposongeza moto wa kigeni mbele za BWANA.

62. Na hao waliohesabiwa kwao walikuwa ishirini na tatu elfu, kila mwanamume tangu huyo aliyepata umri wa mwezi mmoja, na zaidi; kwa kuwa hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli, kwa sababu hawakupewa urithi katika wana wa Israeli.

63. Hao ndio waliohesabiwa na Musa na Eleazari kuhani; ambao waliwahesabu wana wa Israeli katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko.

64. Lakini katika watu hao hapakuwa na mtu hata mmoja wa wale waliohesabiwa na Musa na Haruni kuhani; waliowahesabu wana wa Israeli katika bara ya Sinai.

65. Kwa kuwa BWANA alisema juu yao, Hapana budi watakufa nyikani. Napo hapakusalia mtu mmoja miongoni mwao, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

Hes. 26