Hes. 25:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;

8. akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli.

9. Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.

10. Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia,

11. Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, kwa kuwa alikuwa na wivu kati yao kwa wivu wangu mimi, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu.

12. Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani;

13. tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya Mungu wake, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli.

14. Basi jina la Mwisraeli huyo aliyeuawa pamoja na yule mwanamke Mmidiani, aliitwa Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba zake, katika kabila la Simeoni.

15. Na jina la huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa, aliitwa Kozbi, binti Suri; naye alikuwa kichwa cha watu wa nyumba ya baba zake huko Midiani

16. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

17. Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga;

18. kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.

Hes. 25