Hes. 22:28-41 Swahili Union Version (SUV)

28. BWANA akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?

29. Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.

30. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!

31. Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi.

32. Malaika wa BWANA akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu,

33. punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.

34. Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena.

35. Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.

36. Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.

37. Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi?

38. Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.

39. Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi.

40. Balaki akachinja ng’ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye.

41. Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.

Hes. 22