Hes. 22:22-36 Swahili Union Version (SUV)

22. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

23. Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani.

24. Kisha malaika wa BWANA akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.

25. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili.

26. Malaika wa BWANA akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto.

27. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake.

28. BWANA akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?

29. Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.

30. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!

31. Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi.

32. Malaika wa BWANA akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu,

33. punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.

34. Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena.

35. Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.

36. Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.

Hes. 22