Hes. 22:10-23 Swahili Union Version (SUV)

10. Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,

11. Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.

12. Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.

13. Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana BWANA amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.

14. Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi.

15. Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza.

16. Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie;

17. maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa.

18. Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la BWANA, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.

19. Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua BWANA atakaloniambia zaidi.

20. Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.

21. Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.

22. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

23. Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani.

Hes. 22