21. Kisha Israeli akatuma wajumbe kumwendea Sihoni mfalme wa Waamori, na kusema,
22. Nipe ruhusa nipite katika nchi yako; hatutageuka kando kwenda mashambani, wala kuingia katika mashamba ya mizabibu hatutakunywa maji ya visimani; tutakwenda kwa njia kuu ya mfalme, hata tutakapokuwa tumepita mpaka wako.
23. Lakini Sihoni hakukubali kumwacha Israeli kupita katika mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, akatoka aende kupigana na Israeli jangwani, akafika mpaka Yahasa; akapigana na Israeli.
24. Israeli wakampiga kwa makali ya upanga, na kuimiliki nchi yake, tangu mto wa Arnoni hata mto wa Yaboki, mpaka nchi ya wana wa Amoni; kwa kuwa mpaka wa wana wa Amoni ulikuwa una nguvu.
25. Basi Israeli wakaitwaa miji hiyo yote; Israeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, katika Heshboni, na miji yake yote.