2. Basi Israeli akaweka nadhiri kwa BWANA akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa.
3. BWANA akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma.
4. Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.
5. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.
6. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
7. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.
8. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.
9. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
10. Kisha wana wa Israeli wakasafiri, wakapanga marago Obothi.
11. Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika jangwa iliyoelekea Moabu, upande wa maawio ya jua.
12. Kutoka huko wakasafiri, wakapanga katika bonde la Zeredi.
13. Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.