13. Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea BWANA, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo.
14. Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako.
15. Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea BWANA cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa.
16. Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini).
17. Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, iwe harufu ya kupendeza.
18. Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako.
19. Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa BWANA, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za BWANA kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.
20. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli.
21. Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.