Hes. 16:12-25 Swahili Union Version (SUV)

12. Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi;

13. je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa?

14. Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji.

15. Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao.

16. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni;

17. mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake.

18. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni.

19. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote.

20. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

21. Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.

22. Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote?

23. BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

24. Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu.

25. Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye.

Hes. 16