Hes. 16:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni;

2. nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa;

3. nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA?

4. Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi;

5. kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake.

6. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote;

7. vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu BWANA atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.

8. Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi;

9. Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia;

Hes. 16