26. nao mkutano wote wa wana wa Israeli watasamehewa, na mgeni akaaye kati yao; maana, katika habari za hao wote jambo hilo lilitendeka pasipo kujua.
27. Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi.
28. Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa.
29. Mtakuwa na sheria moja kwa huyo afanyaye neno lo lote pasipo kujua, kwa huyo aliyezaliwa kwenu kati ya wana wa Israeli, na kwa mgeni akaaye kati yao.
30. Lakini mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo amtukana BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
31. Kwa sababu amelidharau neno la BWANA, na kuyavunja maagizo yake; mtu huyo atakatiliwa mbali, uovu wake utakuwa juu yake.
32. Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya Sabato.
33. Hao waliomwona akikusanya kuni wakamleta kwa Musa na Haruni, na kwa mkutano wote.
34. Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa halijasemwa atakalotendwa.
35. BWANA akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote watampiga kwa mawe huko nje ya marago.
36. Basi mkutano wote wakampeleka nje ya marago, nao wakampiga kwa mawe, akafa; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
37. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia,
38. Nena na wana wa Israeli, na kuwaagiza ya kwamba wajifanyie vishada katika ncha za nguo zao, katika vizazi vyao, tena ya kwamba watie katika kila kishada cha kila ncha nyuzi za rangi ya samawi;
39. nacho kitakuwa kwenu ni kishada, ili mpate kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya BWANA, na kuyafanya; tena kwamba msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na macho yenu wenyewe, ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza;
40. ili mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa Mungu wenu.
41. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.