Hes. 15:20-32 Swahili Union Version (SUV)

20. Katika unga wenu wa kwanza wa chenga-chenga mtasongeza mkate uwe sadaka ya kuinuliwa; vile vile kama mfanyavyo sadaka ya kuinuliwa ya sakafu ya kupuria nafaka, ndivyo mtakavyoiinua.

21. Malimbuko ya unga wenu mtampa BWANA sadaka ya kuinuliwa, katika vizazi vyenu.

22. Tena mtakapokosa, msiyashike maagizo hayo yote BWANA aliyomwambia Musa,

23. hayo yote BWANA aliyowaagiza kwa mkono wa Musa, tangu siku hiyo BWANA aliyoleta maagizo, na baadaye katika vizazi vyenu

24. ndipo itakapokuwa, kama ni kosa lililofanywa pasipo kujua, wala mkutano haukuwa na fahamu, ndipo mkutano wote utasongeza ng’ombe mume mmoja mdogo kuwa sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA, pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji, kama amri ilivyo, na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi.

25. Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mkutano wote wa wana wa Israeli, nao watasamehewa; maana, lilikuwa ni kosa, nao wamekwisha leta matoleo yao, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, na sadaka yao ya dhambi pia wameileta mbele za BWANA kwa ajili ya kosa lao;

26. nao mkutano wote wa wana wa Israeli watasamehewa, na mgeni akaaye kati yao; maana, katika habari za hao wote jambo hilo lilitendeka pasipo kujua.

27. Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi.

28. Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa.

29. Mtakuwa na sheria moja kwa huyo afanyaye neno lo lote pasipo kujua, kwa huyo aliyezaliwa kwenu kati ya wana wa Israeli, na kwa mgeni akaaye kati yao.

30. Lakini mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo amtukana BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.

31. Kwa sababu amelidharau neno la BWANA, na kuyavunja maagizo yake; mtu huyo atakatiliwa mbali, uovu wake utakuwa juu yake.

32. Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya Sabato.

Hes. 15