10. Tena utasongeza nusu ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji, kwa sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.
11. Ndivyo itakavyofanywa kwa kila ng’ombe, au kwa kila kondoo mume, au kwa kila mwana-kondoo mume, au kila mwana-mbuzi.
12. Kama hesabu ilivyo ya hao mtakaowaandaa, ndivyo mtakavyofanya kwa kila mmoja, sawasawa na hesabu yao.
13. Wote ambao wamezaliwa kwenu watafanya hayo yote kwa kuandama mfano huo, katika kusongeza sadaka kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.
14. Tena kwamba mgeni amekaa kwenu, au mtu ye yote aliye kati yenu katika vizazi vyenu, naye yuataka kusongeza sadaka kwa moto, na harufu ya kupendeza kwa BWANA; kama ninyi mfanyavyo, na yeye atafanya vivyo.
15. Katika huo mkutano, kutakuwa na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye pamoja nanyi; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo, na mgeni atakuwa vivyo mbele za BWANA.
16. Itakuwa sheria moja na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye nanyi.
17. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
18. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi niwapelekayo,
19. ndipo itakapokuwa ya kwamba hapo mtakapokula katika chakula cha nchi hiyo, mtamsongezea BWANA sadaka ya kuinuliwa.