Hes. 14:21-34 Swahili Union Version (SUV)

21. lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA;

22. kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu;

23. hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24. lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.

25. Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu.

26. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

27. Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo.

28. Waambieni, Kama niishivyo, asema BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;

29. mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung’unikia,

30. hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

31. Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa.

32. Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili.

33. Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani.

34. Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.

Hes. 14