Hes. 14:16-27 Swahili Union Version (SUV)

16. Ni kwa sababu yeye BWANA hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani.

17. Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema,

18. BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.

19. Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.

20. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;

21. lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA;

22. kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu;

23. hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24. lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.

25. Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu.

26. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

27. Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo.

Hes. 14