Hes. 13:12-30 Swahili Union Version (SUV)

12. Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali.

13. Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli.

14. Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi.

15. Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki.

16. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua.

17. Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani,

18. mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi;

19. na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome;

20. nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza.

21. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi.

22. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.

23. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini.

24. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli.

25. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini.

26. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi.

27. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.

28. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.

29. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.

30. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.

Hes. 13