24. Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya BWANA; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema.
25. Ndipo BWANA akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena.
26. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini.
27. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.
28. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.
29. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake.
30. Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.
31. Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi.
32. Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote.