Hes. 11:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.

2. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma.

3. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao.

4. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

5. Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

6. lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.

7. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola.

8. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya.

9. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.

10. Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika.

11. Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu?

Hes. 11