Hes. 1:42-54 Swahili Union Version (SUV)

42. Katika wana wa Naftali, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

43. wale waliohesabiwa katika kabila ya Naftali, walikuwa watu hamsini na tatu elfu na mia nne (53,400).

44. Hao ndio waliohesabiwa, ambao Musa na Haruni na wale wakuu wa Israeli watu kumi na wawili waliwahesabu; walikuwa kila mmoja kwa ajili ya nyumba ya baba zake.

45. Basi hao wote waliohesabiwa katika wana wa israeli kwa kuandama nyumba za baba zao tangu umri wa miaka ishirini na zaidi; wote walioweza kwenda vitani katika Israeli;

46. hao wote waliohesabiwa walikuwa ni watu waume mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini (603,550).

47. Lakini Walawi kwa kuiandama kabila ya baba zao hawakuhesabiwa katika watu hao.

48. Kwa kuwa BWANA alinena na Musa, na kumwambia,

49. Hiyo kabila ya Lawi tu usiihesabu, wala usiitie hesabu yao katika wana wa Israeli;

50. lakini uwaweke Walawi wawe juu ya maskani ya ushahidi, na juu ya vyombo vyake vyote, na juu ya vitu vyake vyote; wao wataichukua hiyo maskani, na vyombo vyake vyote; nao wataitumikia, na kupanga hema zao kwa kuizunguka maskani pande zote.

51. Tena hapo maskani itakapokwenda mbele, Walawi wataishusha; tena hapo maskani itakaposimamishwa, Walawi wataisimamisha; na mgeni atakayekaribia atauawa.

52. Na wana wa Israeli watazipanga hema zao, kila mtu katika marago yake mwenyewe, kila mtu hapo ilipo beramu yake mwenyewe, kama majeshi yao yalivyo.

53. Lakini Walawi watapanga hema zao kuizunguka maskani ya ushahidi pande zote, ili zisiwe hasira juu ya mkutano wa wana wa Israeli; kisha Walawi wataulinda ulinzi wa hiyo maskani ya ushahidi.

54. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.

Hes. 1