1. Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
2. Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema,
3. Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?
4. Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi;
5. kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.
6. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;
7. nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi.
8. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi.
9. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.
10. Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
11. BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani katika habari ya sheria, mkisema,
12. Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye akagusa kwa upindo wake mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula cho chote, je! Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La.
13. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je! Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi.