3. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.
4. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.
5. Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa.
6. Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.
7. Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.
8. Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale.
9. Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga.
10. Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa.