Ezr. 9:7-15 Swahili Union Version (SUV)

7. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo.

8. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu.

9. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.

10. Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako,

11. ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao.

12. Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele.

13. Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, tena umetupa mabaki;

14. je! Tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yo yote, wala mtu wa kuokoka?

15. Ee BWANA, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili. i.

Ezr. 9