1. Ndipo mfalme Dario akatoa amri, na watu wakatafuta katika nyumba ya vyuo vya tarehe, hapo akiba zilipowekwa katika Babeli.
2. Na chuo kimoja kilipatikana huko Akmetha, katika nyumba ya mfalme iliyo katika wilaya ya Umedi, na ndani yake maneno haya yameandikwa ili yakumbukwe.
3. Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi, mfalme Koreshi alitoa amri, Kwa habari ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nyumba hiyo na ijengwe, mahali watoapo dhabihu, na misingi yake ipigwe na kufanywa imara sana; kuinuka kwake kuwe mikono sitini, na upana wake mikono sitini;
4. ziwepo safu tatu za mawe makubwa, na safu moja ya miti mipya; gharama zake zitolewe katika nyumba ya mfalme.
5. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, ambavyo mfalme Nebukadreza alivitoa katika nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu, akavileta mpaka Babeli, na virudishwe, vikaingizwe tena katika hekalu lililoko Yerusalemu, kila kimoja mahali pake, na wewe uvitie katika nyumba ya Mungu.
6. Basi sasa ninyi, Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na hao wenzi wenu wa Kiajemi, mlio ng’ambo ya Mto, jitengeni na mahali pale;
7. iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie; waacheni liwali wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake.