1. Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli.
2. Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia.
3. Wakati ule ule Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakawajia, wakawaambia, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?
4. Ndipo wakawauliza hivi, Majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani na nani?
5. Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, hao wasiwazuie, hata habari ile imfikilie Dario, ndipo jawabu litakapopatikana kwa waraka.
6. Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Dario; na Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzake wa Kiajemi, waliokuwako huko ng’ambo ya Mto,
7. walimpelekea waraka nao; na maneno haya yakaandikwa ndani yake;Kwa Dario, mfalme Salamu sana.
8. Na ajue mfalme ya kuwa sisi tuliingia nchi ya Yuda, tukafika kunako nyumba ya Mungu mkuu, iliyojengwa kwa mawe makubwa, na miti imetiwa katika kuta zake, na kazi hii inaendelea kwa bidii, na kusitawi katika mikono yao.
9. Ndipo tukawauliza wale wazee, tukawaambia hivi, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?
10. Tukawauliza pia majina yao, ili kukuarifu wewe, tupate kuandika majina ya watu waliokuwa wakubwa wao.
11. Wakatujibu hivi, wakasema, Sisi tu watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunaijenga nyumba iliyojengwa zamani sana, yapata miaka mingi, ambayo mfalme mkuu wa Israeli aliijenga na kuimaliza.