2. Ndipo akasimama Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zake makuhani, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na ndugu zake, nao wakaijenga madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili kutoa sadaka za kuteketezwa juu yake, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, mtu wa Mungu.
3. Wakaiweka madhabahu juu ya msingi wake; maana hofu imewashika kwa sababu ya watu wa nchi; wakamtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu yake, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni.
4. Wakaishika Sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa, wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku kwa hesabu yake, kama ilivyoagizwa, kama ilivyopasa kila siku;
5. na baadaye sadaka ya kuteketezwa ya daima, na za mwandamo wa mwezi, na za sikukuu za BWANA, zilizoamriwa na kuwekwa wakfu, na za kila mtu aliyemtolea BWANA sadaka kwa hiari yake.
6. Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la BWANA ulikuwa haujawekwa bado.