Eze. 8:2-13 Swahili Union Version (SUV)

2. Ndipo nikaangalia, na tazama, kana kwamba ni mfano wa moto; tangu mfano wa viuno vyake na chini, moto; na tangu mfano wa viuno vyake na juu, kana kwamba ni mfano wa mwangaza, kama rangi ya kaharabu.

3. Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu.

4. Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika uwanda.

5. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, inua macho yako sasa, uangalie upande wa kaskazini. Basi nikainua macho yangu, nikaangalia upande wa kaskazini, na tazama, upande wa kaskazini wa mlango, ilikuwako sanamu ile ya wivu, mahali pale pa kuingilia.

6. Akaniambia, Mwanadamu, je! Unayaona wanayoyafanya, yaani, haya machukizo makubwa wanayoyafanya nyumba ya Israeli hapa, hata niende zangu mbali na patakatifu pangu? Lakini utaona tena machukizo makubwa mengine.

7. Akanileta hata mlango wa ua; nami nilipoangalia, tazama, pana tundu katika ukuta.

8. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, toboa sasa katika ukuta huu; nami nilipotoboa, tazama, pana mlango.

9. Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa.

10. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote.

11. Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu.

12. Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, BWANA hatuoni; BWANA ameiacha nchi hii.

13. Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda.

Eze. 8